
KITUO CHA TAARIFA CHA KILIMANJARO TELECOM KICHOCHEO CHA MAPINDUZI YA KIDIGITALI KIKANDA
Katika hatua muhimu ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jerry William Silaa, amefungua rasmi Kituo cha Taarifa (Data Center) cha Kampuni ya Kilimanjaro Telecom Co. Limited kilichoko nchini Uganda.
Kituo hicho cha kisasa cha kuhifadhi taarifa kinatarajiwa kuwa kiungo muhimu katika kusambaza huduma za mawasiliano si tu kwa Uganda bali pia kwa mataifa jirani.
Kwa kutumia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unaosimamiwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Kilimanjaro Telecom imepata fursa ya kuunganisha huduma zake kwa ufanisi zaidi, hivyo kuimarisha upatikanaji wa huduma za intaneti zenye kasi na uhakika katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Silaa alieleza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya Tanzania na Uganda katika sekta ya TEHAMA ni chachu ya mapinduzi ya kidijitali barani Afrika. “Mawasiliano ya uhakika na ushirikiano wa kikanda ni nguzo muhimu katika kufanikisha maendeleo ya kidijitali. Kituo hiki ni mfano bora wa mafanikio tunayoweza kuyapata tukishirikiana kama Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema Mhe. Silaa.
Waziri Silaa yuko nchini Uganda kwa ziara ya kikazi ya siku mbili, kufuatia mwaliko rasmi wa Waziri wa TEHAMA na Miongozo ya Kitaifa wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Dkt. Chris Baryomunsi.
Katika ziara hiyo, Mhe. Silaa pia alitembelea Makao Makuu ya Kilimanjaro Telecom Co. Limited, ambao ni kati ya Wateja wakubwa wa huduma za Mkongo wa Taifa, na hapo alipata fursa ya kujionea namna miundombinu hiyo inavyotumika katika kutoa huduma kwa jamii na taasisi mbalimbali nchini humo.
Ziara ya Waziri Silaa inalenga kuimarisha maunganisho ya kimkakati kati ya Tanzania na Uganda katika maeneo ya miundombinu ya TEHAMA, ujenzi wa masoko ya pamoja ya kidijitali, na matumizi ya teknolojia kama nyenzo ya maendeleo jumuishi kwa watu wa mataifa yote mawili.
Mafanikio haya ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongonzwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Tanzania, kuhakikisha kuwa nchi inakuwa kitovu cha TEHAMA kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Aidha jitihada hizi zinadhihirisha dhamira ya Tanzania ya kuchochea maendeleo ya kidijitali kupitia ushirikiano wa kikanda, ubunifu wa teknolojia, na uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu ya mawasiliano.