KIKAO KAZI CHA MSAJILI WA HAZINA CHA ZIKUTANISHA TAASISI 248 ARUSHA
Mashirika ya Umma yapatayo 248 na Mashirika yasiyo ya Umma 58 kupitia kwa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu yamekutana jijini Arusha katika Kikao cha Pili cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu kilichoandaliwa na Msajili wa Hazina.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Mchechu amesema Kikao Kazi hicho kinatarajiwa kufunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani Agosti 28 Mwaka huu katika Ukumbi wa AICC Arusha.
Bw. Mchechu amesema kwa Mwaka huu Kikao hicho kitajikita katika kuzisukuma Taasisi na Mashirika ya Umma kufikiria ili kuweza kuwekeza nje ya nchi ili kuleta maendeleo endelevu nchini.
Amesema Uwekezaji huo nje ya nchi utasaidia nchi kuutawala uchumi hivyo hakuna sababu ya Taasisi za Umma kushindwa kuwekeza nje ya nchi kutokana na ukweli kuwa baadhi ya huduma zinagusa wateja walio nje ya mipaka ya ya Tanzania.
Amesema ili kufanikisha suala la Uwekezaji nje ya nchi, utendaji wa kazi wa Taasisi za Umma unapaswa kubadilika ili kuwa na mawazo mapana yatakaziwezesha kufanya kazi kwa ufanisi na kupata matokeo chanya.
Ameongeza kuwa Taasisi zinapaswa kuwa na mipango ya muda mrefu ili ziweze kuchangia kwenye Mpango Mkakati wa Nchi wa Mwaka 2025 na hawapaswi kusubiri Tume ya Mipango zifanye zenyewe.
Aidha amesema ndani ya miaka mitatu ya kufanyika kwa Kikao hiki mafanikio makubwa yanatarajiwa zaidi kuanzia Mwaka wa Fedha 2024/2025 ambapo zitakuwepo Taasisi za Umma 30 Hadi 40 zitakazoanza kujitegenea na hivyo kupunguza utegemezi na zitaanza kutoa gawio kwa Serikali.