
KAMILISHENI UJENZI WA MINARA KWA WAKATI- CPA MARWA
Wakandarasi wa ujenzi wa minara ya mawasiliano wametakiwa kufanya kazi kwa bidii na kwakuzingatia viwango vya ubora vilivyowekwa ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kuwawezesha wananchi kunufaika na huduma za mawasiliano.
Hayo yalisemwa na Aprili Mosi mwaka huu wakati wa ziara ya kikazi iliyofanywa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania CPA Moremi Marwa aliyoifanya katika maeneo ya Msoro na Bumba Banga Hill, wilayani Kibiti, Mkoa wa Pwani.
Katika ziara hiyo CPA Marwa alipokea taarifa fupi ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa minara chini ya mpango wa UCSAF Phase 8 huku akikisisitiza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutasaidia kuimarisha mawasiliano, hatua ambayo itawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali.
CPA Marwa alisema kuwa minara hiyo inapaswa kuwaka mapema ndani ya muda na kwamba ucheleweshaji wa miradi hiyo unaweza kusababisha athari hasi kwa maendeleo ya sekta ya mawasiliano, na hivyo ni muhimu kwa wote wanaohusika kuhakikisha wanazingatia muda wa utekelezaji.
"Ujenzi wa minara hii ni muhimu sana kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za mawasiliano, tunahitaji kuona miradi hii inakamilika kama ilivyopangwa ili wananchi waweze kufaidi manufaa yake bila kucheleweshwa," alisema CPA Marwa.
Kwa upande wao, Mkurugenzi wa Ufundi, Bw. Cecil Francis na Meneja Mkoa wa kibiashara wa Dar es Salaam Kusini, Bi. Amina Njechele walimhakikishia Mkurugenzi Mkuu kuwa wanafanya kila jitihada kuhakikisha wanawasimamia Wakandarasi ili miradi hiyo inakamilika kwa ubora wa hali ya juu na kwa muda uliopangwa.
Ziara ya CPA Marwa imeongeza morari kwa watekelezaji wa mradi huo, na ni matarajio kwamba hatua hii itaongeza kasi ya ujenzi wa minara hiyo ili kuhakikisha maendeleo ya mawasiliano yanaenda sambamba na mahitaji ya taifa.