info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MIUNDOMBINU YATOA WITO KWA TAASISI NA MASHIRIKA YA SERIKALI KUTUMIA KITUO CHA TAIFA CHA KUTUNZA DATA KIMTANDAO (NIDC) KATIKA UTUNZAJI WA DATA

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, imefanya ziara katika Kituo cha Kutunza Data Kimtandao (Data Centre) kinachoendeshwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania, (TTCL Corporation) na kuridhishwa na uwekezaji wa kisasa uliofanyika katika kituo hicho ambacho ni mhimili wa huduma za kidigitali nchini.

Akizungumza mara baada ya ziara kituoni hapo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Selemani Moshi Kakoso (Mb) aliziomba Taasisi, Mashirika ya Umma na binafsi na Wizara mbalimbali kutumia Kituo cha Kutunza Data Kimtandao (Data Centre) ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za kidijitali nchini.

“Tunaendelea kutoa wito kwa taasisi zote za Serikali na Mashirika kuangalia umuhimu wa kutumia kituo hiki kuhifadhi Data kimtandao ili kumbukumbu (Data) zao ziwe salama na kukifanya kituo kuwa na miradi endelevu ambayo itasaidia kukuza mapato yake”. Alisema Mhe. Kakoso.

Pamoja na hayo, Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, aliishauri TTCL kufanya maboresho zaidi katika kitengo cha utafutaji masoko ili kuvutia ushawishi wa Mashirika ya Umma na hasa yale ya kibinafsi, Wizara mbalimbali na wateja wengine kujitokeza na kutumia Kituo hicho cha Data Centre.

Alisema upo umuhimu mkubwa wa kuwepo kwa kituo hicho na kwamba kutokana na umuhimu huo, TTCL ni lazima ijikite katika kujenga ushawishi wa masoko hasa wa sekta binafsi ili sekta hizo ziweze kutumia fursa hiyo ya huduma za Data Center katika kutunza kumbukumbu zao kimtandao. 

“…Mkurugenzi fanyeni jitihada za uwekezaji, ili muwe na kitengo kizuri cha masoko kiweze kujiuza hasa kwa sekta binafsi, muwe na ushawishi wa kutumia kitengo hiki cha masoko kwa ajili kuvuta wateja,” alisema Mhe. Kakoso (Mb)

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania – TTCL, CPA Moremi Marwa alisema kituo hicho kina umuhimu mkubwa kwa wateja wanaokitumia kwa sasa kwani licha ya uhifadhi taarifa lakini kinazipunguzia gharama za uendeshaji kwa taasisi na makampuni, hasa ya Kifedha, Bima na Mawasiliano.

Alisema taasisi au makampuni yanayotumia kituo hicho yanakuwa na usalama mkubwa wa kuhifadhi taarifa zao, na pia hayana haja ya kuwa na vitengo vikubwa vya IT na vifaa vyake kwani shughuli kubwa hufanywa na wataalam wa kituo cha Data Center.

Alisema faida zingine ambazo hupata mteja wa Data Centre ni pamoja na usalama wa taarifa na ulinzi kwani kituo kinatumia mifumo ya kisasa ya uhifadhi pamoja na kuwa na vyanzo vya uhakika wa umeme zaidi ya vitatu ambavyo uhakikisha taarifa zipo salama muda wote.

Mkurugenzi Marwa alisema kwa sasa Kituo cha Kutunza Data Kimtandao (Data Centre) kinahudumia jumla ya taasisi 211 za Serikali zikiwa taasisi 123 huku za binafsi zikiwa 85, huku akiziomba taasisi, makampuni na watu binafsi kujitokeza kwa ajili ya kupata huduma katika kituo hicho.