info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

KAMATI YA BAJETI ZANZIBAR YAIPONGEZA TTCL KWA UBUNIFU NA USIMAMIZI WA MIRADI

Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar imelipongeza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa juhudi zake katika kuboresha huduma za mawasiliano pande zote za Muungano. 

Pongezi hizo zimetolewa baada ya wajumbe wa kamati hiyo kufanya ziara ya kutembelea ofisi za TTCL leo Agosti 19 mwaka huu na kujionea miradi inayotekelezwa na shirika hilo ambapo Wajumbe hao wameonesha kuridhishwa namna TTCL inavyotekeleza miradi ya mawasiliano ikiwemo kujenga miundombinu ya kisasa inayoliwezesha shirika hilo kutoa huduma bora.

Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar pamoja na mambo mengine imefanya ziara kwa lengo la kujionea shughuli za shirika hilo na kujadili masuala mbalimbali yanayohusiana na huduma za mawasiliano nchini. 

Wajumbe wa kamati hiyo walipata fursa ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya TTCL ikiwa ni pamoja na ujenzi wa minara, upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na namna mkongo huo ulivyounganishwa na Mkongo wa Zanziba ZICTIA ambapo TTCL imongeza njia mbadala ili kuimarisha mawasiliano endapo changamoto ya mkongo kukatika itakapojitokeza.

Aidha wajumbe hao wameelezwa changamoto zinazolikabili shirika hilo na mpango mkakati wa kuboresha huduma za mawasiliano ndani na nje ya nchi. 

Akifanya wasilisho kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mkurugenzi wa Ufundi Mhandisi Cecil Francis amewaeleza Wajumbe hao namna shirika limekuwa likitoa huduma na kutekeleza majukumu yake ya kuhudumia Wateja wa aina mbalimbali kama Kampuni, Taasisi Binafsi, Wateja wa Rejareja, Serikali pamoja na wateja wa Jumla. 

Akizungumza na Waandishi wa habari Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Mwanaasha Juma amesema Kamati hiyo imetembelea Shirika hilo kwa lengo la kujifunza namna shirika linavyotekeleza majukumu yake pamoja na kujua changamoto zinazolikabili.

 “Sisi kama Kamati tumekuja kujifunza na kuona namna ambavyo wenzetu TTCL wamekuwa wakifanya kazi katika maeneo yao lakini pia kuangalia zile taratibu za utendaji wao wa kazi na majukumu waliyonayo” Amesema Mhe. Mwanahasha na kuongeza “Tumejifunza mambo mengi kwa upande wetu, Shirika hili pia limekuwa likifanya kazi kwa upande wa Zanzibar na tumeona kuwa mambo mengi ambayo yamekuwa wakifanywa kwa kushirikiana baina ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Katika hatua nyingine Mhe. Mwanaasha ameipongeza Menejimenti ya TTCL kwa kuendelea kubuni bidhaa na huduma mbalimbali zinazoendana na mahitaji ya sasa ya wateja na kuitaka Menejimenti hiyo kuzigeuza changamoto mbalimbali zinazojitokeza kuwa fursa na kuwa na mipango madhubuti katika utekelezaji wa majukumu yake kwa Wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), CPA Moremi Marwa ameishukuru Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa kufanya ziara katika shirika hilo. Ambapo amesema kuwa ziara hiyo ni ishara ya ushirikiano mzuri kati ya TTCL na Serikali ya Zanzibar katika kuhakikisha huduma bora za mawasiliano zinawafikia wananchi.

Aliongeza kuwa ziara hiyo imetoa fursa kwa TTCL kuwasilisha miradi inayoendelea, changamoto zinazowakabili, na mipango ya kuboresha zaidi huduma za mawasiliano visiwani Zanzibar na kuahidi kuwa TTCL itaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha kuwa malengo ya kuimarisha miundombinu ya mawasiliano yanafikiwa, huku akisisitiza kuwa mawazo na mapendekezo yaliyotolewa na wajumbe wa Kamati hiyo yatasaidia kuboresha utendaji wa shirika hilo.

“Tumefarijika na ujio wa Wajumbe wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar ambao wametutembelea leo kwa ajili ya kujifunza na kukagua namna ambavyo shughuli zetu tumekuwa tukizifanya. Tumepata fulsa ya kufanya wasilisho kwa Kamati ambalo linahusu mambo yetu ya Kiutendaji, Kimkakati na mambo yetu ya Kibiashara, vilevile tumepata baadhi ya mapendekezo na maelekezo kutoka kwa Wajumbe wa Baraza ambayo sisi kama Menejimenti ya TTCL tutayafanyia kazi kwahiyo tunashukuru sana kwa ujio huu na tutaendelea kutoa ushirikiano kwa wenzetu wa upande wa Zanzibar” Amesema CPA Moremi Marwa.