info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

DRC YAIPONGEZA TANZANIA KWA UWEKEZAJI WA KISASA KWENYE MIUNDOMBINU YA TEHAMA

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imeipongeza Serikali ya Tanzania kwa mafanikio makubwa katika uwekezaji wa miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), hasa katika usimamizi wa Kituo cha Taifa cha Utunzaji Data Kimtandao (NIDC) kinachosimamiwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).

Pongezi hizo zilitolewa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa SOCOF, Bw. Prosper Ghislain, wakati ujumbe kutoka DRC ulipotembelea kituo hicho kama sehemu ya ziara yao ya kujadili utekelezaji wa Mradi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) kupitia Ziwa Tanganyika. 

Mradi huo unatarajiwa kuunganisha Tanzania na DRC kupitia Ziwa Tanganyika hadi jimbo la Kalemie, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi wa kidigitali na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.

Akizungumza katika ziara hiyo, Bw. Ghislain alieleza kuvutiwa na ubunifu na teknolojia ya hali ya juu iliyowekezwa katika kituo hicho, akisema Tanzania imeonesha mfano bora wa kuigwa Afrika Mashariki.

“Tumejionea kiwango kikubwa cha uwekezaji na maandalizi ya kisasa ndani ya kituo hiki cha NIDC. Tanzania imeweka msingi imara wa uchumi wa kidigitali ambao ni mfano wa kuigwa katika ukanda wa Afrika Mashariki,” alisema Bw. Ghislain.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Utunzaji Data Kimtandao (NIDC), Bw. Sostenes Malimi, alisema pongezi hizo ni ushahidi wa mafanikio ya sera na uwekezaji wa Serikali katika sekta ya TEHAMA. 

Alibainisha kuwa TTCL kupitia NIDC inaendelea kuboresha mifumo na miundombinu ya mawasiliano ili kuhakikisha huduma bora na salama za uhifadhi wa taarifa zinapatikana ndani na nje ya mipaka ya nchi.

Bw. Malimi aliongeza kuwa mafanikio haya ni matokeo ya dira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoendelea kusukuma mbele Ajenda ya Uchumi wa Kidigitali, huku Tanzania ikijipambanua kama kitovu cha TEHAMA katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Ziara hiyo imeweka msingi mpya wa ushirikiano wa kiteknolojia kati ya Tanzania na DRC, hatua inayotarajiwa kuimarisha mawasiliano, kuboresha upatikanaji wa huduma za mtandao, na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kupitia teknolojia ya mawasiliano.