info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

WAZIRI KAIRUKI ATEMBELEA OFISI ZA TTCL ZANZIBAR, APONGEZA UTENDAJI NA KUAGIZA KUONGEZA KASI

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angella Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), Januari 26, 2026, alifanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) Zanzibar kwa lengo la kujionea utekelezaji wa majukumu ya shirika hilo katika kuwahudumia wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba.

Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Waziri aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohamed Khamis Abdulla, Naibu Katibu Mkuu Bw. Nicholas Merinyo Mkapa pamoja na Viongozi wengine Waandamizi kutoka wizara hiyo.

Akiwasili TTCL Zanzibar, Mhe. Waziri alipokelewa na Meneja Mkaazi wa TTCL Zanzibar, Bi. Nasra Mugheiry, ambaye alimuelezea kwa kina namna TTCL inavyotekeleza majukumu yake ya msingi, hususan katika upanuzi wa huduma za mawasiliano, intaneti ya kasi (Faiba) na uimarishaji wa miundombinu ya TEHAMA kwa lengo la kuhakikisha wananchi wa Unguja na Pemba wanapata huduma bora, salama na za uhakika.

Mhe. Waziri alipata fursa ya kutembelea na kujionea miundombinu mbalimbali ya TTCL ikiwemo mitambo na mifumo ya mawasiliano, ambapo alielezwa namna inavyosaidia kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wateja wa Zanzibar. 

Baada ya ziara hiyo, Waziri alipongeza uongozi pamoja na Wafanyakazi wa TTCL Zanzibar kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuimarisha sekta ya mawasiliano visiwani humo na kuwataka kuongeza bidii katika utekelezaji wa majukumu yao. 

Mhe. Waziri alifanya ziara hii ikiwa ni sehemu ya juhudi za Wizara anayoiongoza za  kufuatilia na kuimarisha utekelezaji wa miradi na huduma za mawasiliano nchini, ikiwemo Zanzibar, kwa manufaa ya wananchi wote.