info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

VIONGOZI TIMIZENI NDOTO YA RAIS SAMIA-KATIBU MKUU KIONGOZI

Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Mashirika na Taasisi za Umma kimefungwa rasmi na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Mpogole Kusiluka.

Akifunga kikao hicho aliwataka Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma kuhakikisha wanatimiza ndoto ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwa na ufanisi kwa kuhakikisha taasisi na mashirika hayo yanafanya kazi kwa ubunifu ndani ya nchi na kimataifa.

Balozi Kusiluka alisisitiza umuhimu wa uongozi bora na uwajibikaji katika kuimarisha utendaji wa mashirika ya umma, ili kuchangia maendeleo ya taifa na kuongeza ushindani wa kimataifa.

Alisema ndoto ya Rais Samia ni kuhakikisha Taifa linakuwa na mashirika yenye ufanisi mkubwa wa viwango vya kimataifa na uwezo mkubwa wa kuchangia katika pato la Taifa.

Aliwasisitiza Viongozi hao kuwa, ni wajibu wa taasisi na mashirika wanayoyasimamia kuandaa na kutekeleza kwa vitendo mkakati wa kitaasisi wa kupambana na rushwa na kwamba hili hilo lifanikiwe ni  muhimu kuimarisha mifumo ya usimamizi ya utendaji wa kazi.

Kuhusu suala la mikataba Balozi Kusiluka aliwataka Viongozi hao kuzingatia sheria kwenye uandaaji wa mikataba, uingiaji na usimamizi wake.

Aidha aliwakumbusha kutimiza wajibu wao katika kutekeleza maazimio walijiwekea ya mwaka 2024 na kwamba  yale ambayo hayakukamilika mwaka 2023 wafanye jitihada za kuyafanyia utekelezaji.

Katika hatua nyingine Balozi Kusiluka alimkabidhi Cheti cha Shukrani Mkurugenzi Mkuu wa TTCL CPA Moremi Marwa ikiwa ni kutambua michango wa shirika hilo kwakudhamini kikao hicho ambapo lilitoa huduma ya Intaneti yenye kasi kubwa huduma ambayo iliwawezesha washiriki kufanya kazi zao kwa haraka na ufanisi mkubwa.

Hii ni mara ya pili kufanyika Kikao kazi kinachowahusisha Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Mashirika na Taasisi za Umma ambapo lengo la Kikao hiki ni kupeana mikakati, uzoefu na kupokea maelekezo yenye nia ya kuyafanya Mashirika hayo kufanya kazi kwa tija zaidi.

.