info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

UTEKELEZAJI WA MRADI WA KUUNGANISHA MKONGO WA TAIFA WA MAWASILIANO NA MIKONGO YA BAHARINI KATIKA PWANI YA MOMBASA NCHINI KENYA WAKAMILIKA

Serikali kupitia Shirika la Mawasiliano Tanzania - TTCL imetekeleza mradi wa kuunganisha mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na mikongo ya Baharini iliyopo katika Pwani ya Mombasa nchini Kenya hivyo kuongeza uhakika wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano hapa nchini na nchi jirani. 

Akizungumza na Waandishi wa habari Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry Silaa wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa ufikishwaji wa mkongo wa mawasiliano katika mpaka wa Tanzania na Kenya (Horohoro), amesema amefanya ziara hiyo kwa ajili ya kuona mafanikio yaliyofikiwa na kwamba baada ya kujiridhisha huduma itaanza kutolewa ifikapo Februari mwaka huu. 

Waziri Silaa amesema serikali imefanikiwa kutekeleza Kilometa 13991 huku lengo likiwa ni kufikisha kilometa 15000 ifikapo mwezi Juni mwaka huu. 

Amesema hayo yatafikiwa kutokana na serikali kufanya uwezeshaji mkubwa kwa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na wizara hiyo kuiwezesha TTCL kufanya utekelezaji wa malengo hayo ya serikali. 

Amebainisha kuwa mkongo wa mawasiliano umeziunganisha Wilaya 109 kati ya Wilaya 139 na kuongeza kuwa Wilaya 30 zilizosalia zinafanyiwa Kazi katika mwaka huu fedha 2024/2025.

Aidha Waziri Silaa amesema Taasisi mbalimbali zipatazo 325,  halmashauri 77 na kituo jumuishi cha forodha kilichopo Horohoro mkoani Tanga tayari vimeunganshwa na mkongo wa mawasiliano na hivyo kuleta chachu katika utoaji wa huduma kwa wananchi. 

" Leo tumekuja hapa kuona kazi kubwa iliyofanyika ya kutengeneza mkongo ambao unaunganisha nchi yetu na Kenya kupitia hapa Horohoro" amesema Waziri Silaa

Amesema utekelezaji huo unafanya mkongo wa mawasiliano kuwa na njia ya Dar es salaam ambapo unaunganisha mikongo 7 ya mawasiliano ya chini ya bahari iliyoko Mombasa hali ambayo itasidia kuimarisha mawasiliano hata kukiwa na hitilafu katika moja ya njia hizo.

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania(TTCL) CPA Moremi Marwa amesema Shirika hilo linaendela kufanya maboresho ya kimkakati yanayolenga kukuza huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kitaifa na kimataifa ili kuingizia Serikali mapato ikiwemo fedha za kigeni.   

Amesema utekelezaji wa Mradi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano  eneo la Horohoro ulianza mwaka 2009 kufuatia maamuzi ya Serikali ya mwaka 2005 ambayo pamoja na mambo mengine yalilenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha Mawasiliano/TEHAMA katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati.

CPA Marwa amesema, kupitia Mpango Mkakati wa Shirika wa miaka mitano 2022/23  2026/27., Shirika limeona umuhimu mkubwa wa kuongeza thamani ya Mkongo wa Taifa kikanda na kimatatifa kupitia kituo cha Horohoro. 

Hivyo maamuzi ya kimkakati yamefanyika ya kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Mikongo ya Baharini iliyopo Mombasa Kenya kama sehemu uendelezaji na upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Maboresho ya kituo cha Horohoro yalifanyika kupitia Mradi wa Mkongo wa Taifa Awamu ya III(2)(i) ambapo kiasi cha Dola za Marekani 135,000 (Shilingi milioni 371.3) bila kodi zilitumika kwa ajili ya vifaa vipya vya Mkongo wa Taifa kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22. 

Aidha utekelezaji wa mradi umekamilika kwenye wiki ya kwanza ya Januari 2025 kwa kuunganisha kituo cha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano cha Horohoro na iColo Data Center iliyopo Mombasa kupitia mkongo wenye urefu wa takribani Kilomita 138.

.