info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL MSHIRIKI NA MDHAMINI WA MKUTANO WA C2C 2024

Shirika la Mawasiliano Tanzania -TTCL litawezesha huduma ya mawasiliano ya intaneti yenye kasi, Mkutano wa Kimataifa wa TEHAMA na Mawasiliano, (Connect 2 Connect Summit 2024) unaotarajiwa kufanyika kuanzia leo tarehe 18 hadi 19 Septemba, 2024, katika ukumbi wa Hoteli ya Gran Melia jijini Arusha. 

Mkutano huo unafunguliwa rasmi na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry Silaa (Mb) ambapo TTCL ni mshirika muhimu kutokana na jukumu lake kuu kama mtoa huduma za mawasiliano ya simu na intanet ya kasi nchini.

Mkutano huu unawakutanisha wataalam, wabunifu, na viongozi wa sekta ya TEHAMA na mawasiliano kutoka duniani kote kujadili maendeleo katika sekta ya Mawasiliano na TEHAMA.

Katika mkutano huu TTCL inabeba jukumu la kuwakilisha Tanzania katika sekta ya mawasiliano kwenye jukwaa la Kimataifa, hivyo ushiriki wake unaonesha dhamira ya serikali ya kuboresha miundombinu ya mawasiliano na kuhamasisha ujumuishaji wa kidijitali nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Mbali na kushiriki mkutano huu TTCL inajipambanua kama mtoa huduma bora wa intaneti kwakudhamini mkutano huo lengo likiwa ni kuwawezesha washiriki wote kutekeleza majukumu yao kwa haraka na ufanisi. 

Udhamini huu ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Shirika wa kuhakikisha maeneo yote muhimu ya Umma na yale ya kimkakati yanawezeshwa na huduma za intaneti yenye kasi kwa matumizi ya wananchi wote katika maeneo mbalimbali kama vile Kumbi za Mikutano, Stendi za Mabasi, Masoko na sehemu mbalimbali za umma za mapumziko.

Kupitia mkutano huu, shirika linatarajia kupata fursa ya kubadilishana mawazo na wataalam wa kimataifa kutoka katika kampuni binafsi, za serikali, na wadau wa ICT ambao wanaweza kuwa washirika katika miradi ya baadaye inayotolewa na TTCL ikiwa ni pamoja na huduma ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.