info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL KUPELEKA HUDUMA ZA MAWASILIANO KATIKA VITUO VYOTE VYA UTALII NCHINI

Shirika la Mawasiliano Tanzania -TTCL limesema kuwa litapeleka huduma za Mawasiliano katika vituo vyote vya Utalii Nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 24, 2024 na Mkurugenzi wa Biashara wa Shirika la Mawasiliano Tanzania Bw. Vedastus Mwita kwa  niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo CPA Moremi Andrea Marwa wakati wa hafla ya uzinduzi wa Pango la kasa la Salaam uliofanyika katika uwanja wa Dimbani Kizimkazi Zanzibar, ambapo Mgeni Rasmi alikuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa TTCL itaendelea kuhakikisha inashiriki katika kuhamasisha shughuli za Utalii Nchini kwa kupeleka huduma ya Intaneti katika maeneo ya vivutio vya Utalii kote Nchini.

"TTCL kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano itahakikisha inatoa huduma inayostahili na ya viwango vya juu kwa gharama nafuu katika maeneo yote ya Utalii Nchini ili kuongeza idadi ya Watalii na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Nchi,"Amesema

Amesisitiza kuwa TTCL itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali zote mbili katika kutekeleza mikakati na mipango mbalimbali ya kupeleka huduma za Mawasiliano hasa ya Intaneti ya kasi katika maeneo mbalimbali nchini na pembezoni mwa mipaka ya Nchi, ili kuhakikisha Serikali inatimiza malengo yake ya kuwahudumia Watanzania wote.

Aidha,amebainisha kuwa TTCL itaendelea kufanya mapinduzi makubwa katika utoaji wa huduma za Mawasiliano Nchini kwa kuzingatia mahitaji ya sasa na ya baadae ya Taifa.

Shirika la Mawasiliano Tanzania-TTCL limeshiriki Tamasha la Kizimkazi 2024 kama wadhamini wakuu kwa kushirikiana pamoja na Benki ya Taifa ya Biashara-NBC ambapo wamedhamini matukio makuu matatu ambayo ni uzinduzi wa pango la kasa (Salaam Cave) uliofanyika katika uwanja wa Dimbani, Fainali ya ligi ya mpira wa miguu (Samia youth cup) utakaofanyika katika uwanja wa Amani na Usiku wa Bongofleva na Zenjifleva utakaofanyika Paje Zanzibar usiku wa tarehe 24 Agosti, 2024.

.