info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

SOCOF YAPONGEZA TTCL KWA UWEKEZAJI KATIKA MIUNDOMBINU YA MAWASILIANO

Ujumbe kutoka Kampuni ya Mawasiliano ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (SOCOF) umehitimisha ziara yake hapa nchini, ikiwa na lengo la kujadili kwa kina utekelezaji wa Mradi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) unaotarajiwa kuunganisha Tanzania na DRC kupitia Ziwa Tanganyika hadi Jimbo la Kalemie. 

Mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kuimarisha mawasiliano ya kikanda na kukuza uchumi wa kidigitali katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Wakati wa ziara hiyo, ujumbe huo ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa SOCOF, Bw. Prosper Ghislain, ulipata fursa ya kutembelea Kituo cha Kitaifa cha Uendeshaji wa Mkongo wa Taifa (Network Operations Centre – NOC) kilichopo jijini Dar es Salaam, pamoja na miundombinu ya kimataifa ya mawasiliano kupitia kampuni ya SEACOM. 

Ziara hiyo iliwapa nafasi ya kujionea jinsi Tanzania inavyosimamia kwa ufanisi miundombinu ya mawasiliano ya kimkakati inayounganisha nchi mbalimbali barani Afrika.

Kupitia ziara hii, Tanzania na DRC zimeimarisha uhusiano wao wa kibiashara na kiufundi katika sekta ya mawasiliano, hatua ambayo inatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma bora za mtandao, kuchochea biashara mtandao na kukuza uchumi wa kidigitali kwa wananchi wa mataifa yote mawili.