info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

MRAJISI WA VYAMA VYA USHIRIKA AGUSWA NA HUDUMA YA MALIPO KWA MKUPUO YA T-PESA

Shirika la Mawasiliano Tanzania – TTCL Corporation limepongezwa kwa ubunifu wake wa kuiona fursa kwa Wakulima na kuanzisha huduma ya Malipo kwa Mkupuo kwa Vyama vya Ushirika nchini.

Pongezi hizo zimetolewa na Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini Dkt. Benson Ndiege alipotembelea Banda la shirika wakati wa Maonesho ya Wakulima (Nane Nane) katika Viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma.

Dkt. Ndiege alisema huduma hiyo imeanzishwa wakati muafaka kwani itakuwa mkombozi kwa Wakulima ambayo itawasaidia kuondokana na kulipa au kupokea fedha kwa mtindo wa ‘kashi’ na hivyo fedha zao zitakuwa salama kutokana na kupitia katika mfumo rasmi.

Alisema kwenye Vyama vya Ushirika kuna watu zaidi ya 500 ambao wanalima mazao yanayofanana hivyo wanapohitaji kulipana huduma hii itawasaidia na kuleta tija zaidi.

"Mfumo huu unaenda kuwasaidia vyama vyote vya ushirika kwani ni njia salama na ya kuaminika na itasaidia katika utendaji kazi", alisema Ndiege

Aidha Dkt Ndiege aliongeza kuwa kutokana na umuhimu wa huduma hiyo upo umuhimu wa kutoa elimu kwa washirika wa Vyama vya Ushirika na kuangalia jinsi huduma hiyo itakavyoenda kuwanufaisha.