info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

MHE. SILAA APONGEZA JUHUDI ZA TTCL KATIKA KUUNGANISHA AFRIKA

Waziri wa  Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe.Jerry Silaa amepongeza juhudi za Shirika la Mawasiliano Tanzania-TTCL katika kuungaisha nchi za jirani Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia na Malawi katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. 

 

Amesema hayo, alipotembelea Banda la TTCL mara baada ya ufunguzi rasmi wa Mkutano wa Connect to Connect ulioanza leo tarehe 18 Septemba, 2024 katika ukumbi wa Hoteli ya Gran Melia jijijni Arusha.

 

Aidha, Mhe. Jerry amelitaka Shirika kuendelea kukamilisha upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenye Wilaya na mradi wa kuunganisha nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo- DRC kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kupitia ziwa Tanganyika Mkoani Kigoma hadi katika jimbo la Kalemie DRC. 

 

Mkurugenzi wa Ufundi wa TTCL Eng.Cecil Francis kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika alipata fursa ya kumuonesha Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe.Jerry Silaa namna Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ulivyounganisha Mikoa, Wilaya na  nchi za jirani  kupitia mipaka ya nchi yetu. 

 

Sambamba na hilo Mhe. Silaa alipata kuona Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano utakapopita wakati wa kuunganisha nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo- DRC kupitia ziwa Tanganyika Mkoani Kigoma hadi katika jimbo la Kalemie DRC.

 

Ili kuhakikisha ubora na uhakika wa huduma, Eng Cecil alimueleza Mhe. Waziri kuhusu Mkongo wa Taifa ulivyounganishwa na Mikongo ya Kimataifa ya Baharini ikiwa ni pamoja na SEACOM, EASSY, na hivi karibuni tutaunganisha 2-AFRICA. 

 

Aidha, juhudi za kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) na Mikongo ya Kimataifa ya Baharini iliyofika katika pwani ya Mombasa Kenya zinaendelea kupitia Kituo cha Horohoro Tanga.