info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

MKURUGENZI MKUU WA TTCL ATEMBELEA TANGA KUKAGUA UJENZI WA MINARA YA MAWASILIANO

Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, amefanya ziara ya kikazi katika mkoa wa Tanga kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa ujenzi wa minara ya mawasiliano vijijini. Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za TTCL kuhakikisha wananchi wa maeneo ya vijijini wanapata huduma bora na za uhakika za mawasiliano.

Katika ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu ametembelea mnara unaojengwa katika Kata ya Kwamkonje, Kijiji cha Kwamkunga (Wilaya ya Handeni) na mnara mwingine katika Kata ya Mkomazi, Kijiji cha Mtindiro (Wilaya ya Korogwe). Ujenzi wa minara hii ni sehemu ya mpango wa upanuzi wa mtandao wa mawasiliano nchini, ili kuimarisha upatikanaji wa huduma za simu na intaneti kwa jamii za vijijini.

Akizungumza katika ziara hiyo, Moremi Marwa ameonesha dhamira ya TTCL ya kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano ili kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wote, hususan wale waliopo maeneo ya pembezoni.

“Tunatambua umuhimu wa mawasiliano katika kuchochea maendeleo ya jamii. Kupitia miradi hii, tunahakikisha kuwa inakamilika kwa wakati na kila Mtanzania anapata fursa sawa ya kufikiwa na huduma za kidigitali,” alisema Marwa.

TTCL inaendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali katika kutekeleza miradi ya mawasiliano vijijini, kwa lengo la kuhakikisha kila kona ya nchi inakuwa na mtandao wa uhakika unaowezesha mawasiliano ya haraka na yenye ufanisi.