info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

CPA MARWA ATOA WITO KWA WANANCHI KUTUNZA MIUNDO MBINU YA MAWASILIANO

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), CPA Moremi Marwa, amefanya ziara ya kukagua mnara wa mawasiliano uliojengwa katika kijiji cha Msomera, wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga. Mnara huo umeleta mabadiliko makubwa katika maisha ya wananchi wa eneo hilo na kuwa chanzo cha huduma ya Intaneti ya kasi ya 4G.

Kupitia ziara hiyo,CPA Marwa aliwahakikishia wananchi kwamba TTCL imejitolea kuboresha huduma zake na kuhakikisha kila mmoja anaweza kufikiwa na teknolojia ya kisasa. "Huduma hii ya Intaneti ya kasi haitaleta tu maendeleo katika mawasiliano, bali pia itawawezesha wananchi kushiriki katika shughuli za kiuchumi zinazotumia teknolojia," alisema Marwa

Aidha, aliwasihi wananchi kuhakikisha wanatunza na kulinda miundombinu hiyo ili uwepo wa huduma hiyo uendelee kuleta manufaa katika jamii. "Ni jukumu letu sote kulinda rasilimali hizi. Ni lazima tuwe na utamaduni wa kutunza miundombinu hii ili iweze kuendelea kufanya kazi kwa muda mrefu," aliongeza.

Mnara huu wa mawasiliano sio tu umekuwa chachu ya maendeleo ya kisasa, bali pia ni mfano wa jinsi teknolojia inavyoweza kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya watu. TTCL inajivunia kuwa sehemu ya mabadiliko haya, ikihakikisha kuwa huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi popote walipo.