TTCL YATOA SEMINA KWA WABUNGE WA KAMATI YA PIC
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Agosti 24 mwaka huu lilitoa semina maalum kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) katika Ukumbi wa Mikutano wa Msekwa Anex uliopo Viwanja vya Bunge Dodoma.
Akitoa Semina hiyo Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Bw. Moremi Marwa amewaeleza wajumbe hao kuhusu mipango ya kibiashara, miradi inayoendelea, na changamoto zinazokikabili shirika hilo.
Katika semina hii Bw. Marwa alieleza mipango ya maendeleo na namna TTCL inavyolenga kuimarisha uwekezaji ili kuongeza ufanisi na tija katika huduma zinazotolewa kwa Wananchi na kuelezea juhudi zinazofanyika katika kuboresha miundombinu ya mawasiliano na kutanua huduma hasa katika maeneo yasiyofikiwa kirahisi.
Aidha Semina hii imekuwa fursa muhimu kwani iliwapa nafasi wajumbe wa kamati kuelewa kwa undani mchango wa TTCL kwenye uchumi wa nchi na kujadili masuala yanayohusiana na uboreshaji wa huduma na uwekezaji wa mitaji ya umma kwenye sekta ya mawasiliano.
Pia, semina hiyo imetoa fursa kwa wajumbe wa PIC kufahamu mchango wa TTCL katika kuimarisha huduma za mawasiliano nchini na namna wanavyotekeleza majukumu yao kwa maslahi ya umma na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wa Kamati hiyo ilipongeza Shirika hilo kwa hatua na maendeleo katika kuboresha huduma na kuimarisha ufanisi katika uendeshaji.
Kamati hiyo pia ilifurahishwa na juhudi za TTCL katika kuboresha huduma kwa wateja na mikakati ya kujiimarisha kwenye ushindani wa soko la mawasiliano.
Pamoja na pongezi hizo Kamati hiyo ililitaka Shirika hilo kuendelea kufanya kazi kimkakati ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya Teknolojia na kuhakikisha huduma zinawafikia Wananchi wengi zaidi hasa maeneo ya vijijini.
Kamati hiyo ilisema kupitia semina hii wamezibaini changamoto zinazolikabili Shirika hilo na kwamba watashirikiana kuhakikisha changamoto hizo zinatatuliwa ili Shirika liweze kufanya kazi kwa ushindani zaidi.